Taasisi ya Usomaji na Maendeleo—Soma kwa ushirikiano na Commonwealth Writers na English PEN wanapenda kuwaalika waandishi na wafasiri wabunifu kutuma maombi ya kushiriki kwenye Warsha ya Ufasiri wa Fasihi ya Kiswahili – Kiingereza, itakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Tarehe 7/11/2016 hadi Tarehe 11/11/2016.
Warsha itaongozwa na Richard Mabala Mwandishi mahiri wa riwaya, hadithi fupi na makala na Dr. Ida Hadjivayanis, Mhadhiri wa Kiswahili na ufasiri wa Chuo Kikuu SOAS Uingereza.
Washiriki wa warsha wafanya tafsiti ya pamoja ya hadithi fupi moja na shairi moja. Waandishi wa tungo hizo watakuweko kujibu maswali yao na kufafanua masuala yenye utata. Warsha hii itatoa fursa ya kushirikiana, kujifunza kwa pamoja na kubadilisdhana uzoefu. Kila mshiriki ataweza kupendekeza tafsiri kuntu ya dhana na hisia kutoka lugha na utamaduni wa Kiswahili kwenda Kiingereza na kujadiliana na wenziwe juu ya changamoto zilizomo katika kufanya tafsiri za aina hii. Washiriki wataweza pia kujifunza nadharia, mbinu za ufasiri na kujiimarisha katika fani hii. Baada ya warsha, kila mshiriki atapewa kazi ya kutafsiri hadithi au shairi moja. Tafsiri hizi zichapishwa hapa Tanzania na Uingereza katika Mkusanyiko wa Fasihi ya Kisasa toka Tanzania/Afrika Mashariki.
Sifa za washiriki:
Muombaji asiwe chini ya miaka 18. Awe raia wa Tanzania au nchi nyingine ya Afrika Mashariki.
Jinsi ya kushiriki:
Fomu ya maombi inapatikana kwenye tovuti ya Soma; www.somabookcafe.com unaweza pia kuipakua na kutuma kwetu kwa njia ya barua pepe kwenda: somabookcafe@yahoo.com.
Mwisho wa kupokea maombi: Tarehe 20/10/2016
Mrejesho:
Maombi yatapitiwa na jopo la waamuzi. Watakaokidhi vigezo watafahamishwa wiki moja kabla ya warsha kuanza.
Mahali:
Warsha itafanyika Mkahawa wa Vitabu Soma/Soma Book Café, Mlingotini Close, Kitalu Na. 53, Mtaa wa Regent, Mikocheni, Dar es Salaam.